Sat, 16 Mar 2024 | 12:27 PM
Dkt. Prosper Mgaya amewasili rasmi Chuoni leo tarehe 14 Machi,2024 na kukutana na Menejimenti ya Chuo. Akizungumza na Menejimenti ya Chuo Dkt.Mgaya amesisitiza dhamira yake ya kufanya kazi kwa kushirikiana kwa weledi na ubunifu ili kutimiza malengo ya Chuo. ‘’NIT ni Chuo cha kisekta, hivyo jamii na Serikali ina matarajio makubwa na Chuo chetu kwahiyo tuna kazi kubwa ya kufanya ili kukidhi matarajio hayo …. Tujipange wote kwa pamoja ili tuweze kusonga mbele na uwezo wa kufanya hivyo tunao”. Dkt. Mgaya amesema kuwa kazi ya kiongozi ni kutambua na kutumia uwezo wa watu alionao na kuendelea kurekebisha mapungufu yao, hivyo amewataka Viongozi wa Chuo kuwatazama watumishi wao katika muktadha huo ili kufanikisha malengo ya Chuo. Amewasihi Viongozi kufanya kazi kwa ushirikiano na kutambua mchango wa kila mmoja kwasababu hakuna anayeweza kufanikisha malengo ya Taasisi akiwa peke yake. Amesisitiza kila mmoja afanye kazi yake kwa uadilifu na juhudi. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 4 Machi 2024 alimteua Dkt. Mgaya kuwa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT). Dkt. Mgaya anachukua nafasi ya Prof.Zacharia Mganilwa ambaye alimaliza muda wake wa utumishi wa umma mwezi Novemba, 2023, na nafasi hiyo kukaimiwa na Dkt. Zainabu Mshana ambaye ni Naibu Mkuu wa Chuo – Mipango Fedha na Utawala, kabla ya uteuzi huo Dkt. Mgaya alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA