Fri, 27 Jun 2025 | 05:41 PM
Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimefanya kikao cha kawaida cha Baraza la Wafanyakazi tarehe 27 Juni, 2025 katika Ukumbi wa Midland Inn View Hotel, Dodoma. Kikao hicho kilitanguliwa na kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika Juni 26, 2025.
Kikao hicho kilifunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, ambaye alikipongeza chuo kwa kuandaa vikao vinavyodumisha ushirikiano wa watumishi na uongozi. Alisisitiza kuwa NIT iendelee kuzalisha wataalamu kutokana na ukuaji wa sekta ya usafirishaji unaoletwa na miradi kama SGR na ongezeko la ndege za ATCL. Aidha, alihimiza ushirikiano na vyuo vya nje kwa ajili ya maendeleo ya kiteknolojia.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo, Prof. Obadia Mbamba, alishukuru Wizara kwa ushirikiano wake unaosaidia ustawi wa chuo. Viongozi wa vyama vya wafanyakazi wa THTU na RAAWU Taifa waliupongeza uongozi wa NIT kwa maandalizi bora ya kikao na kutoa motisha kwa watumishi (incentive) inayoongeza morali ya kazi.
Mkuu wa Chuo, Dkt. Prosper Mgaya, alimshukuru Prof. Kahyarara kwa kuwa mgeni rasmi na kuahidi kuendeleza vikao hivyo kwa kuzingatia sheria na kanuni husika.