Thu, 26 Jun 2025 | 11:29 AM
Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), kupitia Kituo chake cha Kikanda cha Umahiri katika Usalama Barabarani (RCoERS), kimeanza kutoa mafunzo maalum ya usalama barabarani kwa madereva wa magari makubwa ya mizigo, daladala na bodaboda katika Mkoa wa Pwani.
Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo yaliyofanyika tarehe 24 Juni, 2025 katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Kibaha, Mkuu wa Kituo cha Umahiri cha Kikanda cha Usalama Barabarani – NIT, Ndg. Godlisten Msumanje, alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo madereva hao kutekeleza majukumu yao kwa weledi, huku wakizingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kulinda usalama wao pamoja na wa abiria wanaowahudumia.
“NIT imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji nchini kutoa elimu endelevu ya usalama barabarani kwa makundi mbalimbali katika jamii ili kuongeza uelewa wa usalama barabarani kwa watumiaji wote wa barabara,” alisisitiza Ndg. Msumanje.
Mafunzo haya yalianza rasmi tarehe 23 Juni, 2025 na yanatarajiwa kukamilika tarehe 27 Juni, 2025.